Waziri wa Madini Doto Biteko ametoa siku moja kwa Wafanyabiashara wote wa Madini Mkoani Arusha kuhamishia shughuli zao ndani ya Soko na watakao bainika kununua madini nje ya Soko watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni zao na kufikishwa Mahakamani.
Hatua hiyo inafuatia ziara ya kushtukiza ya Waziri Biteko aliyoifanya Sokoni hapo Novemba 13, 2019 na kubaini changamoto za wanunuzi Wakubwa wa Madini kutolitumia Soko hilo na badala yake wameendelea kununua Madini nje ya Soko.
Katika zira yake hiyo, Waziri Biteko ameambatana na viongozi mbalimbaliwa Serikali pamoja na Wizara ya Madini akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Mkoa wa Arusha Jonathan Shanna na wengine.
Aidha, Waziri Biteko amemuagiza Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula kumuondoa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Robert Erick kwa kushindwa kusimamia ipasavyo shughuli za Madini Mkoani humo.
Afisa Madini huyo anadaiwa kuwaachia wafanyabiashara wakubwa wa Madini Mkoani Arusha kufanya biashara ya Madini maofisini mwao tofauti na maelekezo ya Serikali iliyowataka wafanye biashara hiyo kwenye Masoko ya Madini ambapo ofisi nne tu ndizo zilikuwa wazi wakati Soko hilo lina ofisi za wafanyabiashara wakubwa 40 lakini kwa zaidi ya miezi minne hawajahamia katika ofisi hizo.
News
Wafanyabiashara Madini Arusha Wapewa Siku Moja Kuhamishia Shughuli Zao Ndani ya Soko
